JINSI YA KUSHINDA USAILI(INTERVIEW) YA KAZI→ January 24, 2010
Natumaini kwamba hujambo na unaendelea na mapambano ya maisha kwa ujasiri,bila woga wala dalili za kukata tama.Hivyo ndivyo inavyotakiwa.Kumbuka kwamba penye nia pana njia.Jifunze jambo jipya kila siku.Usipoteze muda bure.
Uchumi wa dunia bado haujatengemaa.Bado habari za makampuni kufungwa,kupunguza wafanyakazi,kufilisika na mambo kama hayo,tunazisikia na tutaendelea kuzisikia.Hatujui lini uchumi utarudia hali yake ya kawaida au tuseme ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.Hakuna anayejua kwa hakika.Hata Rais Obama hajui. Kilichobakia hivi sasa ni imani tu kwamba huenda kesho ikawa bora kuliko jana.Imani.
Kwa sababu ya kuyumba huko kwa uchumi,wengi wameshapoteza kazi zao na wengi zaidi wapo mbioni kupoteza.Lakini kupoteza kazi sio mwisho wa maisha.Kwa ufupi ukipoteza kazi uliyonayo hivi leo,huo ni mwanzo wa mbio za kutafuta kazi nyingine.
Kwa maana hiyo wengi wanaopoteza,kuachishwa au kuanza kutafuta kazi hivi leo,wanahitaji mbinu za kushinda mtihani wa usaili(interview). Leo nitaongelea jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya usaili,jinsi ya kujiongoza wakati wa usaili nk.
Kabla sijakuambia ninachotaka kukuambia,naomba nikwambie jambo moja la msingi.Ushindi katika jambo lolote hutokana na jinsi unavyojiamini.Kujiamini hata wakati wa usaili ni jambo la msingi na ambalo lazima ulizingatie.Lakini kumbuka kujiamini hakumaanishi kiburi,majivuno au maringo.Ninaposema kujiamini ninamaanisha kuwa na uhakika na unachokisema na kuonyesha kwamba una uhakika bila majigambo wala kiburi.
Umepata barua au simu kuhusu usaili.Zingatia yafuatayo;
Hakikisha umepata taarifa za kutosha: Mara nyingi upatapo barua au simu inayokuita kwenye usaili,mtu yeyote hujawa na furaha au msisimko wa ajabu.Ni ruksa kufurahi lakini kumbuka kuchukua taarifa muhimu(hususani kama habari hii inakujia kwa njia ya simu) kuhusu mahali utakapofanyiwa usaili(anuani,namba ya chumba,gorofa ya ngapi nk),muda na kama usaili huo utakuwa na watu zaidi ya mmoja au la.Taarifa kama hizo zitakusaidia katika kujiandaa.
Fanya uchunguzi kuhusu shirika/kampuni husika: Kabla ya kwenda kwenye usaili hakikisha kwamba umefanya uchunguzi wa kutosha kuhusu kampuni au shirika husika(research).Wanashughulika na nini,wateja wao ni kina nani,linamilikiwa na nani,lilianzishwa lini na kwa malengo gani.
Kama unamjua mtu au rafiki ambaye aliwahi kufanya kazi katika shirika au kampuni hiyo,mtumie ili kupata taarifa za ndani zaidi.Ufahamu wako kuhusu kampuni au shirika utawaonyesha wanaokufanyia usaili shauku uliyonayo kuhusu kampuni/shirika. Kumbuka tu kutojifanya unajua kupita kiasi.Bakia kwenye kiwango kinachostahili. (more…)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
toa maoni yako kadri uwezavyo.